Nuru FM
Nuru FM
9 March 2026, 9:45 am

Serikali imeweka mifumo na vituo vya kuripoti matukio ya ukatili, na wananchi wanapaswa kuitumia
Na Fredrick Siwale
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amekemea tabia ya baadhi ya wanawake, kutotoa ushahidi katika mashauri yanayohusiana na matukio ya ukatili jambo ambalo linadhoofisha jitihada za serikali katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.
Mh. Kheri ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Wilayani Mufindi na kuongeza kuwa bado wananchi wanatoa ushirikiano mdogo pindi wanapokutana na matukio hayo licha ya serikali kuweka mifumo na vituo vya kuripoti matukio ya ukatili.

Aidha Mh. Kheri amekemea vikali tabia ya kutumia mitandao ya kijamii kuwadhalilisha Wanawake na Watoto jambo ambalo ni kinyume na Sheria.
Mhe. Kheri James amesisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa na ushahidi pale panapotokea ukatili, kwani bila ushirikiano huu jitihada za serikali kupunguza na kuondoa ukatili haziwezi kufanikishwa kikamilifu.
Nae, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, ASP Elizabeth Swai, amewataka wazazi na walezi kulinda watoto hususan nyakati za jioni na usiku, kwani matukio ya ukatili dhidi ya watoto yamekuwa yakijirudia mara kwa mara.
Takwimu za Matukio ya Ukatili mwaka 2026 zilizotolewa na Mkuu wa Idara ya maendeleo ya Jamii Mkoa wa Iringa Bi. Saida Mgeni, zinaonyesha kupungua kwa matukio takribani 350, ikilinganishwa na matukio 400 yaliyoripotiwa miaka miwili iliyopita.
