Nuru FM

Mkataba wa Mil 900 kujenga machinjio Iringa

3 February 2026, 9:36 am

Mstahiki Meya Manispaa ya Iringa akizungumzia mkataba wa machinjio. Picha na Hafidh Ally

Kampuni ya GIPCO Construction Ltd yashinda tenda ya ujenzi wa machinjio ya kisasa mjini Iringa.

Na Hafidh Ally

Manispaa ya Iringa imesaini mkataba wa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 900 na Kampuni ya Jipco kwa ajili ya ujenzi wa machinjio ya kisasa yatakayojengwa katika eneo la Ngelewa, ili kuboresha huduma za uchinjaji na usalama wa afya kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini mkataba huo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, amesema ujenzi wa machinjio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuboresha miundombinu ya huduma muhimu, hususan katika sekta ya mifugo na afya ya jamii.

Sauti ya Ngwada

Amesema machinjio ya kisasa yatasaidia kudhibiti uchinjaji usiozingatia viwango, kuongeza usafi na ubora wa nyama inayofika kwa wananchi, pamoja na kutoa mazingira bora ya kazi kwa wachinjaji na wafanyabiashara wa nyama.

Sauti ya Ngwada

Meneja wa Kampuni ya GIPCO Construction Ltd Ndg. Alexanda Muchunguzi amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huu.

Hafla hiyo ya Utiaji saini imehudhuriwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ndg. Zaina Mlawa, Afisa Kilimo wa Manispaa, Mwanasheria wa Manispaa, Kaimu Afisa Manunuzi wa Manispaa Bi. Jema Monge na viongozi wa Kampuni ya GIPCO Construction Ltd wakiongozwa na Meneja Ndg. Alexanda Muchunguzi.