Nuru FM

Bonde la Rufiji laongeza mapato kwa 50%

3 December 2025, 7:07 pm

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James akizungumza katika Uzinduzi wa Bodi ya Bonde la Mto Rufiji. Picha na Adelphina Kutika

“Ukusanyaji wa Mapato umesaidia kupima utendaji kazi wa watumishi wa Bodi hiyo”

Na Adelphina Kutika

Bodi ya Tisa ya Bonde la Maji Rufiji imefanikiwa kuongeza mapato ya ndani kutoka shilingi bilioni 2.4 mwaka 2022/2023 hadi kufikia zaidi ya shilingi bilioni 3.6 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 50.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Kumi ya Bonde hilo katika ukumbi wa Bodi ya Maji Rufiji mkoani Iringa, Mwenyekiti wa Bodi iliyomaliza muda wake, Bi. Naomi Lupimo, amesema ongezeko hilo la mapato ni ushahidi wa uwajibikaji, ubunifu na usimamizi madhubuti wa rasilimali za bonde.

Sauti ya Mwenyekiti

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bonde la Rufiji (RBWB), David Mkyala, amebainisha kuwa Tanzania ina jumla ya mabonde tisa ya maji, huku Bonde la Rufiji likishika nafasi ya kwanza kwa ukubwa likiwa na eneo la kilomita za mraba 183,791, sawa na asilimia 20 ya eneo lote la nchi.

Sauti ya Mkurugenzi

Akizindua Bodi hiyo ya Kumi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James amesifu Bodi ya Tisa kwa kutekeleza majukumu yake kwa weledi mkubwa na kuonyesha mfano wa kuigwa na mabonde mengine nchini huku akitoa rai kwa Bodi mpya kuendeleza misingi iliyojengwa ili kuhakikisha usimamizi endelevu wa vyanzo vya maji.

Sauti ya Kheri

Baadhi ya wajumbe waliomaliza muda wao, akiwemo Bi. Lucy Joseph Tewele, amesema wametekeleza majukumu yao kwa jitihada kubwa, wakijivunia kufanikiwa kuwafikia wananchi katika ngazi za chini kwa asilimia 90, lengo likiwa ni kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali.

Sauti ya Wajumbe

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa kuwatambulisha wajumbe wa Bodi ya Kumi, ambao wametakiwa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuimarisha ushirikiano na jamii katika uhifadhi wa rasilimali za maji.