Nuru FM

Wafanyabiashara waaswa kukatia bima biashara zao.

26 November 2025, 7:15 am

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, akizindua rasmi kampeni ya “NIC Kitaa”. Picha na Moses Mbwambo

“Bima hizo zitawasaidia kupata fidia endapo utakutana ana majanga yatakayoharibu biashara”

Na Godfrey Mengele

Wafanyabiashara wanaojishughulisha na shughuli za sekta isiyo rasmi ikiwamo bodaboda, mamalishe, wauza mitumba na makundi mengine wametakiwa kujiunga na huduma za bima ili kujilinda na majanga yanayoweza kuathiri biashara na maisha yao ya kila siku.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Masoko wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Karimu Meshack, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya NIC Kitaa mkoani Iringa, ambayo itatekelezwa kwa muda wa siku saba akibainisha kuwa bima ni nguzo muhimu katika ustawi wa kiuchumi.

Sauti ya Mkurugenzi NIC

Kwa upande wake, Meneja wa NIC Mkoa wa Iringa, Paul Mkumbo, amesema kampeni hiyo inalenga kufikisha huduma za bima karibu zaidi na wananchi, ikiwemo maeneo ya vijijini kupitia mawakala na mifumo ya malipo kwa njia ya simu.

Sauti ya Meneja

Akizindua kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema kuwa Serikali kupitia NIC itaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika huduma za bima nchini.

Sauti ya RC Iringa

Kheri amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa bima, ikiwa ni sehemu ya ajenda ya kitaifa ya kujenga taifa lililo salama kiuchumi, kijamii na kimfumo.

Pia Mhe. Kheri amepongeza NIC kwa kuendelea kutoa huduma za bima nchini kwa takribani miaka 62, akisisitiza kuwa uzoefu huo mkubwa umeiwezesha taasisi hiyo kuwa chombo muhimu cha kulinda mali na maisha ya wananchi dhidi ya majanga mbalimbali kama moto, ajali na majanga mengine yanayosababisha hasara.

Kwa mujibu wa takwimu za NIC, zaidi ya wananchi 300,000 tayari wamenufaika na mpango wa NIC Kitaa tangu uanze kutekelezwa, huku juhudi zikiendelea kuhakikisha huduma hizo zinawafikia watu wengi zaidi nchini.