Nuru FM
Nuru FM
18 November 2025, 2:02 pm

“Wajasiriamali wanapaswa kuunganishwa na taasisi za kifedha kwa lengo la kuwainua kichumi”
Na Adelphina Kutika
Wataalamu waliofadhiliwa na shirika la Campaign for Female Education (CAMFED) nchini Tanzania wameiomba Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) kuwasaidia kuwaunganisha na taasisi za kifedha, wajasiriamali pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati, ili kuongeza mitaji na kukuza biashara zao.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa chama cha wataalamu hao (CAMA Professionals), Bi Zena Ally ambapo pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na shirika la Camfed katika kuwawezesha wasichana hao kiuchumi, bado mikopo wanayoipata haikidhi mahitaji halisi ya biashara wanazozifanya, hasa katika sekta ya kilimo.
Akijibu ombi hilo, Mkurugenzi wa Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC), Bi Mwajuma Hamza, amesema taasisi yake ipo tayari kushirikiana na wataalamu hao katika maeneo yenye tija, ikiwemo mafunzo ya ujasiriamali, upatikanaji wa masoko na uwezeshaji wa mitaji.
Awali, Mkurugenzi wa Miradi kutoka CAMFED Tanzania, Bi Anna Sawaki, alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kuwawezesha wataalamu hao kujifunza kutoka kwa wadau mbalimbali wa biashara kuhusu mbinu bora za uwekezaji na usimamizi wa miradi.
Hata hivyo Mkutano huo ulihudhuriwa na wataalamu kutoka mikoa mbalimbali nchini, wakiwemo wajasiriamali vijana waliopitia programu za CAMFED, wakijadiliana namna bora ya kukuza uchumi wa wanawake kupitia ushirikiano na taasisi za kifedha na biashara.