Nuru FM
Nuru FM
20 August 2025, 11:15 am

Malezi ni mchakato wa kumtunza, kumuelekeza, kumuongoza na kumuelimisha mtoto hadi anapofikia umri wa kujisimamia mwenyewe.
Na Joyce Buganda
Wazazi na walezi mkoani Iringa wametakiwa kushirikiana kwa pamoja katika Malezi ya watoto ili kuwasaidia katika ukuaji wa maadili mema katika jamii.
Hayo yamezungumzwa na Mratibu wa Programu Jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto PJT MMMAM mkoa wa Iringa Martin Chuwa kwenye kikao kilichowajumuisha wadau mbalimbali wa watoto na kuongeza kwa kusema ni vema wazazi wakajitahidi kupata muda wa kukaa na watoto wao ikiwa ni pamoja na kucheza nao ili kuwafanya wakue katika utimilifu.
Chuwa amesema ni vema wazazi na walezi wakawatengea watoto wao sehemu za wazi kwa ajili ya michezo ya asili kwa maeneo ya nyumbani ili kuwajenga Zaidi kiakili, na kifikra.
Kwa upande wao baadhi ya wazazi Manispaa ya Iringa wameeleza kuwa watoto wanapokuwa katika malezi mazuri huishi katika kufuata maadili waliyofundishwa na wazazi na walimu shuleni.
PJT MMMAM ni programu jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto wa kuanzia miaka 0 mpaka miaka 8 yenye afua tano ambazo ni lishe, afya, malezi yenye muitikio, ujifunzaji wa awali na ulinzi na usalama.