Nuru FM
Nuru FM
11 August 2025, 12:29 pm

Katika kukabiliana na magonjwa ya Mlipuko kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Kidilo, Shirika la World Vision Tanzania limejenga vyoo vya kisasa.
Na Adelphina Kutika
Zaidi ya wanafunzi mia mbili wa Shule ya Msingi Kidilo, iliyopo kata ya Kihanga Wilaya ya Iringa, wameondokana na kuugua homa ya magonjwa ya matumbo na kipindupindu baada ya kujengewa matundu ya vyoo kumi na mbili.
Akizungumza shuleni hapo ,Mkuu wa shule hiyo Mwl Mchina Mkeng’e amesema ujenzi huo wenye thamani ya shilingi milioni tisini umewezeshwa na Shirika la World Vision , ambalo limekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa watoto vijijini.

Nao Baadhi ya wazazi wa wanafunzi hao wameeleza kuwa kabla ya mradi huo, watoto wao walikuwa wakipatwa na maradhi ya mara kwa mara, jambo lililoathiri pia mahudhurio yao shuleni.
Mwakilishi wa Shirika la World Vision Tanzania ambaye anasimamia mradi wa afya , lishe , usafi wa mazingira na maji kata ya kihanga Neema Temba, alifanya ukaguzi wa usafi ulifanyika shuleni hapo, ukiangazia vyoo na usafi wa mazingira ametoa wito kwa walimu, wanafunzi na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanatunza miundombinu hiyo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Shule ya Msingi Kidilo ni miongoni mwa shule inayotegemewa na wakazi wa kijiji cha Kidilo kwa ajili ya watoto wao kupata elimu, lakini kwa muda mrefu ilikuwa na matundu sita tu ya vyoo, hali ambayo ilikuwa ikihatarisha afya za wanafunzi kutokana na msongamano na uchafuzi wa mazingira.
