Nuru FM
Nuru FM
7 August 2025, 4:11 pm

Uboreshwaji wa miundombinu ya shule imetajwa kuwa sababu ya kukuza kiwango Cha ufaulu Mashuleni.
Na Adelphina Kutika
Mkoa wa Iringa umepokea jumla ya Shilingi bilioni 7.5 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kutatua changamoto za uchakavu wa miundombinu ya elimu na kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule.
Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha maafisa elimu, maafisa manunuzi, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa shule, wakandarasi pamoja na wakuu wa vitengo mbalimbali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Kheri James amesisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa miradi ya uboreshaji wa elimu kupitia Mpango wa BOOST.
Aidha Mkuu huyo amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa kuhakikisha fedha zilizotolewa zinatumika ipasavyo kutekeleza na kukamilisha Ujenzi uliokusudiwa kwa wakati ili thamani ya fedha ionekane Wazi Kupitia Miradi hiyo ili ikawafae Wananchi.
Kwa upande wao, Maafisa Manunuzi, Wahandisi wa ujenzi, Wakuu wa Shule na Wakandarasi, wamepongeza hatua hiyo ya serikali na kueleza changamoto kadhaa zinazowakabili katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi .
Hata hivyo kufuatia kikao hicho mkuu huyo ameagiza miradi yote inayotekelezwa kupitia BOOST katika halmashauri zote mkoani Iringa inapaswa kukamilika ifikapo Novemba 30, 2025, huku akiwataka washiriki wote wa kikao kazi hicho kuhakikisha wanazingatia maadili ya kazi, thamani ya fedha na ubora wa kazi zinazotekelezwa.