Nuru FM

Wananchi Iringa walaani Mtoto kutupwa dampo

7 August 2025, 10:48 am

Viongozi wa Mtaa, Kata na Maafisa Kutoka jeshi la polisi wakichukua mwili wa Mtoto aliyetupwa. Picha na Zacharia Nyamoga

Tukio hilo la kusikitisha limebainika baada ya vijana wanaokusanya plastiki kugundua mwili huo, uliokuwa umefichwa chini ya takataka.

Na Hafidh Ally

Wananchi wa Mtaa wa Ngome Kata ya Kihesa Manispaa ya Iringa wamelaani tukio la mwili wa Mtoto mchanga kutupwa katika dampo la taka karibu na soko la Ngome.

Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya wananchi wa eneo hilo wamesema kuwa matukio ya watoto kutupwa hayakubaliki huku wakiwataka kuwekwe ulinzi maeneo ya dampo ili kuwakamata watakaofika katika maeneo hayo wakati wa usiku.

Sauti ya Wananchi

Aidha wamewataka wanawake kutojihusisha na ngono zembe jambo linalopelekea kubeba ujauzito na kufanya  ukatili huo ambao ni kinyume na maadili ya kibinadamu huku wakitaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua stahiki.

Sauti ya Wananchi

Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngome, Festo Mtiauli, amesema kuwa tayari taarifa zimefikishwa kwa mamlaka husika huku akiwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama katika kutoa taarifa zitakazosaidia kufanikisha uchunguzi.

Sauti ya Festo

Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Kihesa Geofrey Mgimwa amesema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa hiyo na amekiri kuwa matukio hayo kwa sasa yamekuwa machache kwa sababu wanatoa elimu kwa jamii huku wakiwaonya watu kutofanya matukio ya kutupa watoto.

Sauti ya Mtendaji

Tukio hilo la kusikitisha lilibainika baada ya vijana wanaokusanya plastiki katika eneo hilo kugundua mwili huo, uliokuwa umefichwa chini ya takataka na kufunikwa kwa suruali chakavu.