Nuru FM
Nuru FM
12 July 2025, 12:12 pm

Moto huo ulizuka majira ya saa 8 usiku ambapo mali mbalimbali za wafanyabiashara zikiteketea na kusababisha hasara.
Na Ayoub Sanga
Wafanyabiashara wa Soko la Mashine Tatu, lililoko katikati ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, wamejikuta katika majonzi makubwa baada ya soko hilo kuteketea kwa moto mkubwa usiku wa kuamkia leo Julai 12, 2025..
Wakizungumza na Nuru FM baadhi ya wafanyabiashara hao wamesema kuwa Moto huo ambao chanzo chake bado hakijafahamika rasmi, umeharibu sehemu kubwa ya soko hilo la bidhaa za malimbichi, na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara waliokuwa na maduka na vibanda katika eneo hilo.

Mashuhuda wanasema moto ulianza majira ya saa tano usiku na ulienea kwa kasi kubwa kutokana na kuwepo kwa bidhaa nyingi zinazowaka kwa urahisi, ikiwemo mbao, majani, na plastiki.
Kwa upande wake Raphael Ngulo mwenyekiti wa masoko Manispaa ya Iringa amesema kuwa jumla ya wafanyabiashara waliokuwa ndani ni 429 na vibanda vya nje 86 ambavyo vimeteketea kwa moto nab ado hawajafanya tathmini kujua hasara imekuwa kiasi gani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa Benjamini Sitta amesema kuwa Serikali itafanya tathimini kujua madhara yaliyojitokeza na chanzo cha moto huo baada ya kufanya uchunguzi wa kina.

Hakuna taarifa rasmi kuhusu majeruhi au vifo, lakini hasara ya mali inakadiriwa kuwa kubwa. Uongozi Wilaya ya Iringa umeahidi kushirikiana na vyombo vya usalama na taasisi husika katika kuchunguza tukio hilo na kuwasaidia waathirika.
