Nuru FM
Nuru FM
8 July 2025, 8:33 pm

Katika mipango yake ya kuboresha huduma, Serikali kupitia Wizara ya Afya, ina utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.
Na Zaitun Mustapha na Rogasia Kipangula
Uongozi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa umesema kuwa serikali imefanikiwa kuboresha huduma za afya hasa kuwepo na ICU, vifaa vya kisasa sambamba na uwepo wa madaktari bingwa.
Hayo yamezungumzwa na Afisa habari Hospital ya Rufaa Mkoa wa Iringa Bi. Zainab Mlimbila na kuongeza kuwa kuna mabadiliko yaliyofanywa katika kipindi cha miaka mine ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluh Hassan jambo linalosaidia kurahisisha utoaji wa huduma za afya.

Anasema deni walilonalo kwa Rais na watanzania kwa ujumla ni kutoa huduma bora za afya kwa kuzingatia weledi, maadili na miiko ya kitaaluma ya watoa huduma za afya sambamba na kuzingatia utoaji wa huduma nzuri kwa mteja, na matumizi ya lugha ya staha na ya faraja kwa wateja.
Anataja baadhi ya huduma ambazo zilikuwa hazitolewa katika hospitali lakini sasa zinatolewa kuwa ni pamoja na huduma za CT Scan ambayo ni aina ya uchunguzi wa picha za mwili unaozingatia mionzi.

Kwa upande wao baadhi ya Wananchi Manispaa ya Iringa wameelezea mabadiliko ambayo wameyaona katika hospitali hiyo ikiwemo vitanda na majengo ya kisasa sambamba na vifaa vyote vya kisasa kwa magonjwa ya watoto, wazee na wajawazito.
Aidha wananchi hao wameiomba serikali kuwapunguzia gharama za matibabu kwani wengi wao wanashindwa kuzimudu.
