Nuru FM
Nuru FM
23 June 2025, 7:06 pm

Idadi kubwa ya wanaume wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili kwa kunyimwa tendo la ndoa, lakini usiri ndio unapelekea kufikia hatua mbaya hata kufanya mauaji ya wenza wao au kujikatisha uhai wenyewe.
Na Adelphina Kutika
Wanaume wanaokumbwa na Ukatili wa kijinsia majumbani, ikiwamo kunyimwa tendo la ndoa na wake zao wametakiwa kuvunja ukimya na kuripoti matukio hayo katika dawati la jinsia ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi kukomesha unyanyasaji huo.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Iringa, Wakili Moses Ambindilwe, katika semina maalum iliyowakutanisha wajumbe wa mabaraza ya usuluhishi ya kata, wenyeviti wa mitaa na watendaji wa kata ya Nduli, kueleza kuwa lengo la semina hiyo ni kuwajengea uwezo viongozi hao juu ya masuala ya utawala bora na mbinu za kushughulikia vitendo vya ukatili katika jamii.

Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Iringa kutoka kitengo cha dawati la jinsia na watoto, Bi. Loveness Mayingu, amewataka wanaume wasiogope kuripoti ukatili wa namna hiyo, kwani sheria haimbagui mtu kwa misingi ya jinsia.

Katika semina hiyo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kilimahewa, Dorah John Jonathan, amesema kikao hicho kimetoa mwanga mkubwa kwa viongozi wa mitaa na kata katika kushughulikia matukio ya ukatili, hasa dhidi ya watoto, kwani wazazi wengi wamekuwa wakiwatelekeza watoto wao kwa kujikita zaidi katika shughuli za kiuchumi.
Naye Diwani wa Kata ya Nduli, Mh. Bashiri Mtove, amemshukuru Wakili Ambindilwe kwa kutoa elimu hiyo muhimu na kusisitiza kuwa viongozi wa mitaa sasa watakuwa mabalozi wa sheria kwa wananchi wa Nduli, hasa katika kuhamasisha haki na usuluhishi wa migogoro kwa njia ya kisheria.