Nuru FM
Nuru FM
13 June 2025, 11:09 am

Wanawake wamehamasishwa kujitokeza kwa wingi kupambania nafasi za uongozi ili kuingia kwenye ngazi za uamuzi.
Na Hafidh Ally
Kuelekea uchaguzi Mkuu wa Okt 2025, Wanawake Mkoani Iringa wametakiwa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili kupata wawakilishi watakaosemea changamoto zao.
Hayo yamezungumzwa na Mfaume Juma Gomangulu Katibu UVCCM Wilaya ya Iringa Vijijini na kuongeza kuwa Jumuiya yao imekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wanawake na vijana kujua umuhimu wa kuwa kiongozi.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake Chadema Jimbo la Iringa Mjini Bi. Yasinta Mwinuka Chama chao kimewapa kipaumbele wanawake kushika nafasi mbalimbali katika uongozi ili kujenga ustawi katika jamii.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi Manispaa ya Iringa wamesema kuwa kwa sasa kumekuwa na mwamko mkubwa kwa wanawake kujitokeza kugombea katika nafasi za uongozi tofauti na hapo awali.
Takwimu zilizotolewa na Kituo cha Demokrasia Tanzania kupitia ripoti hiyo zinaonyesha idadi ya sasa ya wanawake katika Bunge ni 144, ambapo 26 pekee kati yao walichaguliwa moja kwa moja huku 113 wakichaguliwa kupitia viti maalumu wawili kutoka Zanzibar na Watatu wakichaguliwa na Rais ikionyesha idadi ndogo zaidi ya wanawake wanaochaguliwa moja kwa moja kutoka kwenye majimbo.