Nuru FM
Nuru FM
10 June 2025, 11:26 am

Kutokana na uwepo wa baridi kali katika baadhi ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wananchi wameaswa kuchukua hatua za kiafya ili kuepuka magonjwa yanayosababishwa na hali hiyo.
Na Zaitun Mustapha Na Catherine Soko
Wananchi Mkoani Iringa wametakiwa kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha baridi kali ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya hewa ikiwemo Nimonia.
Hayo yamezungumzwa Dokta Ihonde wa Kituo cha Afya Ngome Kilichopo Manispaa ya Iringa na kuongeza kuwa kuna sababu zinapelekea wananchi wengi kupata magonjwa mbalimbali ya mfumo wa upumuaji kama vile kikohozi, mafua, mafindofindo na emonia katika kipindi hiki cha msimu wa baridi kali.
Aidha Dkt. Ihonde amewataka wananchi kuvaa nguo nzito, kuvaa barakoa na kula vyakula vyenye vitamin C na ikiwezekana kufika katika kituo cha afya ili kupatiwa matibabu.
Dokta huyo ameshauri watu kuepuka mazingira ya baridi, kuvaa mavazi ya kukinga mwili kama makoti mazito, soksi, kofia na gloves nzito za vitambaa au uzi kabla ya kutoka.
Amesema watoto wachanga na wazee wanaweza kupata matatizo ya kupungukiwa na joto mwilini ambayo kitaalamu huitwa ‘Hypothermia’ ambayo husababisha vifo, hivyo daktari huyo amewataka watu kuchukua tahadhari.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi Manispaa ya Iringa wamesema kuwa wanavaa masheta mazito, na kupata vyakula vya moto ili kuepukana na magonjwa katika kipindi hiki cha baridi.