Nuru FM

Elimu ya matumizi ya nishati yafika Iringa

2 June 2025, 8:12 pm

Meneja wa EWURA kanda ya kati Hawa Lweno akizungumza kuhusu nishati safi. Picha na Adelphina Kutika

Elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ina lengo la kutunza mazingira katika Jamii.

Na Adelphina Kutika

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kanda ya kati, imeendelea na jitihada zake za kuelimisha umma kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa mama lishe, waendesha bodaboda, na wasambazaji wa gesi mkoani Iringa.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja wa EWURA kanda ya kati Hawa Lweno, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia viwango vya usalama katika usambazaji na matumizi ya gesi ya kupikia (LPG), akibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kulinda maisha na mali za wananchi.

“Ni muhimu kila mdau wa mnyororo wa usambazaji wa gesi kuhakikisha anafuata taratibu na miongozo ya usalama” alisema Lweno.

Naye mwakilishi kutoka Wakala wa Vipimo mkoa wa Iringa, Richard Kimario, amewasihi mawakala wa gesi kuhakikisha wanakagua mitungi kabla ya kuiingiza sokoni, akibainisha kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kudhibiti malalamiko ya upungufu wa gesi na kuhakikisha uzito.

“Mitungi isiyokaguliwa ni hatari kwa mlaji na inaweza kusababisha madhara makubwa, tunataka kila bidhaa inayofika kwa mlaji iwe salama na yenye ubora unaostahili,” alisema Kimario.

Kwa upande wao Washiriki wa mafunzo hayo wamesema elimu itawawezesha kuboresha huduma zao huku wakichangia katika ulinzi wa jamii dhidi ya athari za matumizi yasiyo salama ya gesi.

Hata hivyo Mafunzo hayo ni sehemu ya mikakati ya EWURA kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama kwa ajili ya kuchochea maendeleo endelevu na kulinda mazingira.