Nuru FM
Nuru FM
29 May 2025, 3:18 pm

Ujenzi wa barabara ya Makombe-Kitanewa utaenda kuyaunganisha majimbo mawili ya Kalenga na Ismani na kukuza uchumi wa wananchi.
Na Adelphina Kutika
Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Jackson Kiswaga ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Makombe-Kitanewa yenye urefu wa KM 21.3 inayojengwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa gharama ya Shilingi Milioni 414 katika kata ya Kihanga tarafa ya Kiponzero kwenye Halmashauri ya wilaya ya Iringa.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa TARURA wilaya Jabir Barnabas amesema utekelezaji wa mradi huo umefanyika kwa awamu lengo likiwa kuunganisha mawasiliano majimbo mawili kati ya Jimbo la kalenga na Jimbo la Isimani.
Amesema ujenzi wa mradi huo umefanyika kwa gharama zitokanazo na Bajeti za mwaka wa Fedha 2021/2022, 2022/2023 na 2023/2024.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga amesema Barabara hiyo ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa kwenye suala la maendeleo na Serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.