Nuru FM
Nuru FM
12 April 2025, 1:08 pm

Na Adelphina Kutika
Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, imefanikiwa kujenga mabirika matano ya kunyweshea mifugo na vituo vya kuchota maji safi ya kunywa kupitia mradi wa REGROW, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa vyanzo vya maji katika bonde hilo.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Naomi Lupimo, wakati akiwasilisha taarifa kwa vyombo vya habari Mkoani Iringa juu ya mafanikio Waliyopata katika kipindi cha miaka minne Kupitia uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akibainisha kuwa serikali imeonyesha dhamira thabiti ya kuboresha sekta ya maji.
Aidha amesema serikali imeonyesha dhamira thabiti ya kuboresha sekta ya maji, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa mabirika ya kunyweshea mifugo, hatua inayosaidia wananchi na mifugo katika bonde hilo.

Sambamba na hayo Lupimo amesema kuwa, katika kipindi hicho cha miaka minne Bodi ya Maji Bonde la Rufiji imefanikiwa kuongeza mapato ya ndani kutoka asilimia 57 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 90 mwaka 2024, hatua inayochangia katika maendeleo ya sekta ya maji katika eneo hilo.
Katika hatua Nyingine Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Mhandisi Florence Mahay, ameeleza kuwa katika utoaji wa vibali vya matumizi ya maji, bodi imeanzisha utaratibu wa kutoa vibali kupitia kikao cha maandishi na kusaidia wananchi kupata huduma ya maji kwa wakati na kuepusha ucheleweshaji, hatua ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa jamii.
Hata hivyo Miradi hii inadhihirisha juhudi za serikali katika kuboresha huduma za maji na kulinda vyanzo vya maji kwa ajili ya maendeleo endelevu ya wananchi na mazingira katika Bonde la Rufiji.