

4 March 2025, 10:50 am
Na Frank Leonard
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa kimekanusha taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Steven Mhapa inayodai majina ya madiwani na wabunge waliopo madarakani sasa yatakuwa miongoni mwa majina matatu yatakayorudishwa kwenye mchakato wa kusaka majina ya watakaoiwakilisha CCM kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.
Katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichofanyika hivi karibuni mjini Iringa, Mhapa amenukuliwa akisema madiwani na wabunge hao ni lazima watakuwa sehemu ya wana CCM watatu watakaorudishwa katika kura za maoni za chama hicho kwa ajili ya kupigiwa kura.
Akitangaza msimamo wa CCM mkoa wa Iringa kuhusiana na kadhia hiyo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, Daudi Yassin amesema Kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Iringa imepokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa na kuongeza kuwa kauli hiyo sio msimamo wa CCM mkoa wa Iringa na ni kauli yake mwenyewe binafsi.
“Tunapenda kuweka wazi kwamba kauli hiyo si msimamo wa Chama Cha Mapinduzi bali ni mawazo yake binafsi. CCM haijatoa mwongozo wa aina hiyo na haukubaliki,” alisema Yasin.
Daudi amesema kuwa Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikifuata kanuni na taratibu zimewekwa na unapofika wakati wa uchaguzi wagombea wote wanajadiliwa kwa sifa zao kupitia vikao husika.
Kutokana na hilo alisema, Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Iringa imewataka viongozi wa chama na wanachama kujiepusha na matamko yenye utata yanayoweza kusababisha taharuki miongoni mwa wanachama na jamii kwa ujumla.
“CCM imesisitiza kuwa inaendelea kuzingatia misingi ya demokrasia, huku ikihakikisha mchakato wa uteuzi wa wagombea unafanyika kwa haki na uwazi kulingana na katiba na kanuni za chama” alisema.
Kauli hiyo ambayo ilichapishwa na kutangazwa na baadhi ya vyombo vya habari hususani mitandao ya kijamii na kusambaa kwa kiasi kikubwa imesababisha mkanganyiko na taharuki miongoni mwa wana CCM na wananchi kwa ujumla ambao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu siasa mkoani Iringa.
MWISHO