

25 February 2025, 12:26 pm
Na Adelphina Kutika
Tume ya Taifa na Mpango wa Matumizi ya Ardhi imeanzisha mchakato wa kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kijiji cha Iwungi, kilichopo katika kata ya Uhambingeto, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara, Msimamizi wa Zoezi la Kuandaa Mpango wa Matumizi ya Ardhi, Emmanuel Magembe, amesema kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuhifadhi chanzo cha maji cha bwawa la Mwalimu Nyerere, sambamba na kutoa fursa kwa wananchi wa kijiji hicho kuelezea changamoto zinazowakumba, ikiwemo migogoro ya ardhi.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Uhambingeto, Jumanne Khalid Tembo, alisema kuwa mpango huo umeongeza urahisi katika kupata maeneo ya maziko, ambapo awali walikuwa wakikumbana na changamoto kubwa ya ukosefu wa maeneo rasmi ya maziko.
Wananchi wa Kijiji cha Iwungi pia wameonyesha kuridhika na mpango huo huku wakieleza kuwa umeondoa migogoro ya ardhi hasa kati ya wakulima na wafugaji.
Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika Kijiji cha Iwungi chenye wakazi zaidi ya 178 unalenga kuboresha matumizi ya ardhi na kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto za ardhi na maendeleo ya kijiji hicho.
MWISHO