Nuru FM

CCM Iringa wataja sababu za kuunga mkono Rais Samia kugombea 2025

30 January 2025, 10:00 am

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Salim Abri Asas na viongozi wengine wa CCM katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 48 ya CCM. Picha na Hafidh Ally

Na Hafidh Ally

Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa kimesema kuwa sababu ya mkutano Mkuu wa CCM Taifa Kupendekeza Jina la Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea pekee katika nafasi ya Urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi hasa kwenye miradi ya maendeleo.

Hayo yamezungumzwa na MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Salim Abri Asas katika sherehe ya ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 48 ya CCM iliyofanyika katika Kijiji cha Ng’uruhe wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa na kuongeza kuwa ilani ya CCM imegusa katika utoaji wa huduma za kijamii kama afya, elimu na miundombinu.

Sauti ya ASAS

Akizungumza katika uzinduzi huo, MNEC Asas alisema CCM inaendelea kuadhimisha miaka yake ya kuzaliwa kwa kuwaletea wananchi maendeleo halisi na sio maneno matupu.

Katika hotuba yake, Asas alifafanua kuwa chama tayari kimefunga mjadala wa mgombea wa urais kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM umeazimia kwa kauli moja kuwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ndiye mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku Dk. John Nchimbi akichaguliwa kuwa mgombea mwenza.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kilolo Mh. Justin Nyamoga amewapongeza wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa kwa kupendekeza jina la Samia Suluhu Hassan huku akiishukuru serikali kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa barabara katika Wilaya ya Kilolo.

Sauti ya Nyamoga

Amesema wanatarajia ifikapo mwaka 2027 watatatua changamoto ya miundombinu ya barabara za kilolo mpaka Kijiji cha Kitowo na ujenzi wa sekondari katika kijiji cha Pomerini.

Sauti ya Nyamoga

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilolo, John Kiteve na viongozi wengine mbalimbali walitambua mchango mkubwa wa Rais Dk Samia katika maendeleo ya nchi, hususan katika sekta za maji, elimu, afya, miundombinu, kilimo, viwanda, biashara na utalii.

Ilielezwa kuwa kata ya Ng’uruhe imepata mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Sh Bilioni 1.6, pia, uwekezaji katika sekta ya chai, miti na mazao ya chakula na biashara ukisisitizwa kama sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha maisha ya wananchi.

“Sisi wana Kilolo tunatambua mchango wa Dk. Samia, na ahadi yetu ni moja—tutamlipa kwenye sanduku la kura uchaguzi utakapofika,” alisema Kiteve.