Nuru FM

DC Linda awapa wiki moja wazazi kuwapeleka shule wanafunzi

14 January 2025, 10:48 am

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dkt. Linda Salekwa akizungumza wakati akikagua mahudhurio ya wanafunzi shuleni. Picha na Sima Bingilek

Na Sima Bingilek

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dkt. Linda Salekwa ametoa wiki Moja kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka shule wanafunzi wote waliochaguliwa kujinga na masomo kwa mwaka 2025.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mheshimiwa Dkt. Linda Salekwa alipokuwa akikagua mahudhurio ya siku ya kwanza ya wanafunzi kwa mwaka 2025 na kuongeza kuwa mpaka Jan 20 endapo wazazi hawatawapeleka shule wanafunzi hatua kazi zitachukuliwa dhidi yao.

“ Natoa wiki moja kuanzia tarehe 13 Januari 2025 Wazazi na walezi hakikisheni wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na masomo katika Wilaya ya Mufindi wanaenda Shuleni, tarehe 20Januari, siku ya jumatatu tutafanya msako nyumba kwa nyumba, lengo ni kuhakikisha Ndoto za Mheshimiwa Rais zinatimia za wanafunzi kusoma bure na kupata elimu bora ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu bora ya Madarasa na vifaa”

Aidha amewataka walimu kuwapokea wanafunzi Shuleni hata kama hawana sare au michango yoyote lengo ni kupata elimu, hivyo sare isiwe kikwazo cha kuwazuia wanafunzi wasipokelewe Shuleni.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mheshimiwa Dkt. Linda Salekwa amewatembelea wanafunzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Upendo ambayo imepangiwa wanafunzi 234 wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2025, na Shule Mpya ya Sekondari ya Amali ambayo imepangiwa wanafunzi 36.

Kuhusu uandikishaji wa Awali Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mheshimiwa Dkt. Linda Salekwa amezipongeza Halmashauri za Wilaya ya Mufindi Kwa kuendelea kuandikisha wanafunzi wa Awali ambapo kwa Halmashauri ya Mji Mafinga jumla ya wanafunzi 2109 wakiwemo wanafunzi 7 wa mahitaji Maalumu wameandikishwa.

MWISHO