Shirika la DSW kutoa huduma rafiki za afya ya uzazi Iringa
18 November 2024, 7:44 pm
Na Dorice Olambo
Ili kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma rafiki za afya ya uzazi na maendeleo kwa vijana Shirika la DSW limetambulisha mradi wa Reproductive Equity Strategy in Tanzania (REST) Mkoani Iringa.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa mradi wa huo Mkoani Iringa Mkurugenzi wa DSW Tanzania Peter Owaga ameeleza kuwa mradi huo unatazamia kuongeza uelewa mzuri kwa vijana na wadau kuhusu mipango ya kitaifa ya masuala ya afya.
Aidha ameongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kufanyika kwa kipindi cha miaka mitatu huku maeneo yatakayoanza kwa utekelezaji ni pamoja na halmashauri ya manispaa ya iringa na wilaya ya Iringa kwa kata chache zilizopewa kipaumbele na mkoa.
Mwantumu Dosi ni Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii manispaa ya Iringa amesema mradi huo utawasaidia vijana juu ya masuala ya afya uzazi ,ukatili wa kijinsia na kuwajengea vijana kujitambua.
Hata hivyo Shirika hili lisilo la kiserikali la DSW Tanzania linatekeleza miradi katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Arusha ,Iringa ,Morogoro na Mbeya.
MWISHO