Takwimu za kilimo kusaidia kupambana na njaa ifikapo mwaka 2030
8 November 2024, 11:35 am
Na Hafidh Ally
Serikali inatarajia kufanya Utafiti wa Kilimo, uvuvi na ufugaji Ili kuendana na Milengo ya Milenia ya Maendeleo endelevu ya kupambana na Njaa kabla ya mwaka 2030.
Hayo yamezungumzwa na Kamisaa wa sensa ya watu na makazi Bi. Anna Makinda katika Hafla ya kufunga mafunzo ya siku 14 ya wadadisi na wasimamizi 178 wa Kilimo wa mwaka 2023/24 katika Chuo Cha Afya Manispaa ya Iringa.
Makinda amesema kuwa Wadadisi na wasimamizi hao wanajukumu la kuangalia Takwimu za uzalishaji kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi katika Jamii zao kwa Kuzalisha kwa takwimu sahihi Ili kuongeza uzalishaji na kufanya nchi kuwa kwenye ulimwengu wa mataifa yenye mipango katika uzalishaji kwa kutumia takwimu.
“Niwaambie vijana wangu Roho na uhai wa nchi unategemea takwimu sahihi kwani hata wakulima wakitaka kulima itawasaidia kujua ni mbolea kiasi Gani inahitajika katika shamba la ukubwa kiasi Fulani, na baada ya hapo nitapata mavuno gunia ngapi” Alisema Makinda
Alisema Baada ya Utafiti huo Jamii itaweza kupata miradi ya maendeleo katika Jamii kwani wataangalia wapi penye uhitaji Ili paweze kupewa kipaumbele kutokana na takwimu watakazoziwasilisha.
Naye Mtakwimu Mkuu kutoka Zanzibar Kasimu Salim Ally Alisema kuwa Mafunzo Kama hayo yanaendelea visiwani Zanzibar huku akiwataka Washiriki kutimiza wajibu wao Ili kufikia lengo la utafiti ambao wamefundishwa.
Awali Mtakwimu Mkuu wa serikali Bi Albina Chuwa amebainisja kuwa kitendo cha Kuandaa takwimu za kilimo, uvuvi na ufugaji kitasaidia Kukusanya sera za kuboresha sekta hizo.
Alisema Katika Utafiti wa pili kufanyika kupitia Shirika la FAO duniani walikubaliana kuwa ikifika mwaka 2030 kuwe hakuna njaa katika mataifa yote.
“Utafiti huu utasaidia kuiambia serikali ni wapi tumefikia katika kupambana na Njaa kabla ya mwaka 2030 na niwajulishe kuwa Kilimo kinachangia asilimia 26 ya uchumi wa Tanzania, na Ili tupime kilimo hiki ni lazima kuwe na utafiti na kupima kilimo tunacholima Kama kina tija” Alisema Bi. Albina.
Kwa upande wao baadhi ya Washiriki wa Mafunzo hayo ambao ni Wadadisi na wasimamizi Kilimo wa mwaka 2023/24 wamesema kuwa kupitia sensa ya watu na makazi wataweza Kutekeleza majukumu Yao na kuhakikisha wanaandaa takwimu ambazo zitasaidia kukuza sekta ya Kilimo, uvuvi na ufugaji.