DC Linda azindua Taasisi ya TK Movement
5 November 2024, 11:15 am
Na Fredrick Siwale
Vijana Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Wametakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi na Maendeleo katika Sekta ya Kilimo kufuatia serikali kutoa zaidi ya Milioni 500 katika sekta hiyo.
Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Dkt.Linda Salekwa wakati wa uzinduzi wa taasisi ya Vijana ya TK Movement Wilayani Mufindi na kuongeza kuwa Serikali imetoa Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya Kilimo cha umwagiliaji Mtula ,ambapo Vijana wakichangamkia fursa hiyo wanaweza kujikwamua kiuchumi.
Aidha Linda amesema kuwa kupitia mradi wa Kilimo ni wakati sahihi kwa TK Movement kuungana na serikali kwa katika kupambana na masuala ya udumavu na ukatili.
Katibu wa TK Movement Mkoa wa Iringa, Shaban Wisandara ,amesema lengo la TK Movement ni kuhamasisha Vijana kutumia fursa zilizopo, kujiajiri na kujipatia vipato halali mfano Kilimo ,biashara na ufugaji nyuki.
Mratibu wa TK Movement Zabron Lufyagile ,amesema hadi sasa Wilaya imekwisha sajili Vijana zaidi ya 2,500 katika mfumo rasmi wa TK APP katika Kata zote 36.
MWISHO