Nuru FM

Vijana Iringa kujiinua kiuchumi kupitia mikopo ya Halmashauri

31 October 2024, 10:54 am

Vijana wakiwa katika mahojiano na Nuru FM kuhusu Fursa za mikopo ya Halmshauri. Picha na Ayoub Sanga

Na Shaffih Kiduka, Halima Abdalla, Zahara Said na Shahanazi Subeti

Siku chache baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kutangaza utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, baadhi ya wananchi Manispaa ya iringa wamesema kuwa watatumia fursa hiyo kujiinua kiuchumi.

Wakizungumza na Nuru FM baadhi ya wananchi hao wamesema kuwa mikopo hiyo itawasaidia katika kukuza biashara zao huku wakiwataka watakaobahatika kupata mkopo huo kurejesha kwa wakati ili na wengine waweze kunufaika na fursa hiyo.

Sauti ya Wananchi

Aidha wameitaka serikali kutoa elimu ya namna ya kuitumia mikopo hiyo kujiendeleza kiuchumi na kuweka utaratibu utakaosaidia kuwafikia wahusika wengi ili wanufaike.

Sauti ya Wananchi

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Dkt Festo Dugange amesema mikopo ya Halmashauri ya asilimia 10 itokanayo na mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inatarajiwa kuanza kutolewa kabla au ifikapo Novemba 30, 2024 ili kuwanufaisha walengwa wa mikopo hiyo.

Sauti ya Dugange

Serikali imekwisharekebisha sheria na imeshapitia Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za Mwaka 2019 na marekebisho yake ya mwaka 2021 na kutoa Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za Mwaka 2024.

MWISHO