Mzabuni atekelekeza mradi wa nyumba ya mwalimu Ndolezi
22 October 2024, 11:01 am
Na Fredrick Siwale
Wananchi wa Mtaa wa Ndolezi uliopo Kata ya Boma Halmashauri ya Mji Mafinga wameiomba Serikali kuwatumia wazabuni wa ndani kusimamia miradi ya maendeleo ili kuepukana na ucheleweshaji wa kukamilisha Miradi.
Hayo yamezungumzwa na baadhi ya wananchi wa Mtaa huo kufuatia kusimama kwa mradi wa Ujenzi wa nyumba ya Mwalimu wenye thamani ya shilingi milioni 100 baada ya kutelekezwa na Mkandarasi zaidi ya miezi miwili na kutokomea kusiko julikana.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Tawi la Ndolezi Bw. Lenard Chavala amesema kuwa kinachosababisha zoezi la ujenzi wa jengo hilo ni kutokuwa na fedha za kuendesha zoezi hilo huku wakiiomba serikali kumtafuta mkandarasi ili kumalizia jengo hilo.
Mhe.Justis Kisoma Diwani wa Kata ya Boma Halmashauri ya Mji Mafinga amesema mradi wa nyumba ya Mwalimu Shule ya Sekondari Ndolezi ambao unadaiwa kutelekezwa upo Halmashauri ya Mji Mafinga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa .
Mhe.Kisoma amesema mradi wa nyumba ya Mwalimu ya two in one ulianza Ujenzi wake Agosti 05,2024 na ulipaswa kuwa umekamilika Oktoba 18, 2024 mwaka huu.
Mwenyekiti wa kamati ya bodi ya Shule ya Sekondari Ndolezi Bi.Hongera Swenya ambaye ndiye msimamizi wa Shule pamoja na Afisa elimu Sekondari Halmashauri ya Mji Mafinga Stephen Shemdoe hawakuwa tayari kuzungumza sakata hilo.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mji Mafinga Bi.Fedelica Myovella alipotafutwa kwa njia ya simu yake ya mkononi alidai atafuatilia mwenendo wa ujenzi wa jengo hilo.
Mkandarasi aliyetekeza mradi huo aliyefahamika kwa jina la Hamisi Mkurupale tayari amekwishalipwa kiasi cha shilingi milioni 5.3 kati ya shilingi milioni 100 alizotakiwa kulipwa.