TCRA yataka hisabati kutumika katika uchumi wa kidigitali
4 September 2024, 10:59 am
Na Adelphina Kutika
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka Walimu wa Hesabu kuwaandaa wanafunzi na vijana kujikita katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) ili kupata fursa ya kushiriki maendeleo ya Dunia katika zama hizi za kidijiti.
Hayo yamebainishwa na mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dr Jabir Bakari katika Mafunzo ya Muda Mfupi kwa Walimu wa Hisabati Tanzania Yaliyofanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa(MUCE) Mkoani Iringa na kusema kuwa hesabu ni msingi wa sayansi na teknolojia, na katika ulimwengu unaobadilika haraka wa teknolojia, uchumi wa kidijiti unakuwa injini muhimu ya ukuaji wa kiuchumi.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, Afisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Iringa, Hansi Mgaya, amewataka wakuu wa shule za kuhakikisha wanakuwa na klabu za Hisabati ili kufanya vizuri katika somo hilo.
Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Deusdedit Rwehumbiza, amesema walimu wa hisabati wanapaswa kuwa na jukumu la kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa hayo muhimu kwa ajili ya mafanikio ya baadaye.
Mwenyekiti wa (CHAHITA,) Dk Said Sima, amesema mafunzo hayo yanalenga walimu wa hisabati wanakuwa na uwezo wa kuingia katika uchumi wa kidijiti na kuwasaidia wanafunzi wao kufanya vyema.
Hata hivyo Chama cha Hisabati Tanzania (CHAHITA), huwakutanisha wataalamu hao kutoka mikoa yote nchini kwa malengo mbalimbali, ikiwa na kutoa mafunzo kwa walimu wa hisabati ili kuongeza ujuzi na maarifa yao katika kufundisha somo hilo .
MWISHO