Mradi wa HEET kutatua changamoto ya upungufu wa hosteli MUCE
3 September 2024, 9:33 am
Ukosefu wa hosteli katika kada za elimu hapa nchini Tanzania imekuwa ni changamoto inayowakabili wanafunzi wengi jambo linalopelekea kushindwa kutimiza malengo yao.
Na Adelphina Kutika
Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) wameishukuru serikali kuwaletea mradi wa (HEET) unaokwenda kutatua changamoto ya ubakaji na wizi kwa wanafunzi wanaoishi nje ya hosteli.
Wakizungumza kwa niaba ya wanafunzi Rais wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) Steven Mgalla na Makamu wake Remisha Gastoni Milazi mara baada ya hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa majengo manne kupitia mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (Heet) wenye thamani ya shilingi bilioni 14.8 na kampuni ya Kitanzania ya Dimetoclasa Real Hope Limited and Mponera Construction wamesema wanafurahishwa na mradi huo kwa sababu unakwenda kuwasaidia kupata hosteli .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa(MUCE) Prof. William Anangisye amesema kuwa mradi huo unakwenda kuchangia katika maeneo muhimu ya uvumbuzi, maendeleo ya kiuchumi na umuhimu wa soko la ajira, kwa kuwekeza katika miundombinu inayohitajika kwa ufundishaji na utafiti wa kisasa .
Rais wa chuo hicho Prof. Deusdedit Rwehumbiza amesema mradi huu unakwenda kutatua changamoto kubwa zaidi ya hosteli kwa wanafunzi takribani 6,200.
Dickson Mwipopo ni mkurugenzi wa kampuni ya Kitanzania ya Dimetoclasa Real Hope Limited and Mponera Construction ameomba viongozi kuhakikisha wanatoa kazi wazawa kwa asilimia100 ili kuongeza uchumi wa taifa letu na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
MWISHO