Madiwani Mafinga Mji wahoji uwepo maduka ya dawa karibu na hospitali
20 August 2024, 9:57 am
Madiwani Mafinga mji wamekazia Marufuku ya maduka binafsi ya dawa kuwa karibu na viunga vya hospitali za umma kuwa yanapaswa kuwa umbali usiopungua mita 500 kutoka hospitali ilipo sababu ikitajwa kuwa maduka hayo ya dawa yanahusika katika kuchochea upungufu wa dawa na vifaa tiba kwenye hospitali za umma.
Na Hafidh Ally
Siku chache baada ya serikali kuagiza Wamiliki wa maduka ya dawa za binaadamu kutoweka maduka karibu na hospitali au zahanati, madiwani wa Halmashauri ya Mafinga Mji Mkoani iringa wametaka agizo hilo litekelezwe.
Wakizungumza katika kikao cha madiwani halmashauri ya mafinga Mji, Diwani wa Kata ya Changarawe Mh. Lazaro Sanga na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mafinga Mji Rejinant Kivinge wamesema kuwa ni muda sasa toka agizo hilo litolewe lakini bado halijafanyiwa kazi.
Akizungumzia kuhusu Wamiliki wa maduka ya dawa za binaadamu kuweka maduka yao karibu na watoa huduma za afya, Dr. Bonivenja CHitopela Mganga Mkuu wa Mafinga Mji amesema kuwa bado hawajapokea rasmi waraka wa kuyaondoa maduka hayo.
Amesema kuwa wamiliki wa maduka binafsi ya dawa wanatakiwa kuweka maduka yao umbali wa mita 300 kutoka hispitali ya rufaa mkoa na mita mia 3 kutoka hospitali ya Wilaya.
Hivi karibuni Aliyekuwa Waziri wa afya Mh.Ummy Mwalimu alitoa agizo la kuondolewa kwa maduka yote ya dawa ambayo yapo mita 500 ndani ya eneo la hospitali za Serikali kwa kile kinachodaiwa kuhujumu upatikanaji wa dawa katika hospitali hizo.
MWISHO