ASAS aonya dhidi ya uongozi wa matajiri
5 August 2024, 3:26 pm
Na Frank Leonard
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas, amewaonya wanachama wa CCM kuhusu hatari ya kukumbatia wenye fedha kunyakua uongozi, akihofia kwamba wasio nacho wanaweza kukosa fursa hata kama wana sifa bora zaidi.
Asas ameahidi kuendelea kukemea vitendo vya rushwa katika michakato ya kupata viongozi kupitia chama hicho akisema kuvifumbia macho vitendo hivyo ni kukipasua chama hicho.
“Tukinyamaza na kuvifumbia macho vitendo vya rushwa, chama hiki kitageuka kuwa cha viongozi wenye fedha au matajiri tu,” alisema.
Akizungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Kilolo, Asas alisisitiza kuwa CCM ni chama cha wakulima na wafanyakazi, na akasema fedha haipaswi kufanywa kila kitu katika kupata viongozi.
Aliwaonya wanachama dhidi ya kutengeneza makundi ya kuwabeba wenye fedha katika michakato hiyo ya kutafuta viongozi, akisema wasio na kitu wanatengenezewa mazingira ya kuogopa siasa na uongozi.
“Kuruhusu chama kuongozwa na watu wenye fedha tu kunaweza kuwapotezea wananchi imani na kupunguza ushiriki wao katika mchakato wa kidemokrasia,” alisema.
Katika hatua nyingine, Asas alitoa msaada wa simu janja 148 kwa ajili ya usajili wa wanachama kidigitali katika kata zote za wilaya ya Kilolo.