Nuru FM

MNEC Asas awaonya watia nia wanaoanza kampeni kabla ya muda

5 August 2024, 12:20 pm

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM ya wilaya ya Mufindi. Picha na Frank Leonard

Na Frank Leonard, Mafinga

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas amewakemea watia nia wa nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama hicho, akisema mbali ya kujifanyia kampeni kabla ya muda, wanajijenga wao badala ya kujenga chama.

Akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM ya wilaya ya Mufindi kupitia utaratibu wake wa kila mwaka wa kukutana na viongozi hao, Asas alisema:

“Taarifa zilizopo huko mitaani ni kwamba watu wanajiandaa watashindaje wao kama wao kupitia chama ambacho hawajui na hawataki kujua kitashindaje.

Alisema tabia hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kutengeneza rushwa na makundi ya uchaguzi na kuleta athari kwa chama ikiwa ni pamoja na mipasuko iliyosababisha katika baadhi ya maeneo, kipoteze kwa wapinzani.

Asas alisema uongozi halisi unahitaji maadili, uaminifu, na kujitolea, na haupaswi kupatikana kwa ushawishi au kununuliwa kwa fedha kama inavyofanyika kwa bidhaa za masokoni.

“Uongozi bora unatokana na uwezo wa kuongoza kwa mfano, kuhamasisha wengine, na kutoa maamuzi yenye maadili, si kwa sababu ya rushwa,” alisema.

Alisema katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwakani baadhi ya watia nia wameanza kushindana kwa kutoa rushwa ya kati ya Sh 50,000 na kuendelea kama njia ya kuwarubuni wajumbe ili muda ukifika basi wawe katika nafasi nzuri ya kushinda.

“Nipo tayari kukosolewa kama nasema uongo, asimame mwana CCM yoyote aseme kama nachosema kuhusu chaguzi za baadhi ya watu tunaowatafuta kwa ajili ya kutuwakilisha katika chaguzi mbalimbali hazifanyiki kama mnada, huko ndiko tulikofika,” alisema.

Akilia na watia nia hao Asas alisema yupo tayari kuachia ngazi uongozi alionao kuliko kuendelea kuona chama chake katika mkoa wake wa Iringa kinaharibiwa na rushwa inayosababisha makundi hayo.

Alisema ni muhimu kwa wanachama wote kufuata kanuni na taratibu za uchaguzi kwa haki na uwazi ili kuhakikisha kuwa viongozi wanaochaguliwa ni wale wenye uwezo na nia ya kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.

Katika hatua nyingine Asas ametoa msaada wa simu janja 36 kwa chama hicho wilaya ya Mufindi alizosema zitumike kwa ajili ya usajili wa wanachama kidigitali katika kata zake zote.