PM Majaliwa awafuta kazi vigogo Iringa
9 July 2024, 10:19 am
Na Frank Leonard
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kusimamishwa kazi mara moja Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Emanuel Sigachuma na Ofisa Elimu Sekondari wa halmashauri hiyo Nelson Milanzi, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili na kufikishwa mahakamani.
Wawili hao pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo mstaafu, Laini Kamendu wanatuhumiwa kushindwa kutekeleza wajibu wao na kusababisha kuwepo kwa mashaka ya matumizi ya zaidi ya Sh Milioni 700 za ujenzi wa bwalo la shule mpya ya sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Iringa ya Lugalo.
Kiasi hicho cha fedha ni sehemu ya zaidi ya Sh bilioni tatu zilizotolewa na serikali kupitia mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kujenga katika kila mkoa shule moja ya sekondari ya wasichana ya mkoa.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa shule hiyo inayojengwa katika Kata ya Mbigili wilayani Kilolo na ambayo imeanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano mwaka huu, mhandisi wa halmashauri hiyo alisema ujenzi wa bwalo hilo ambao umefikia zaidi ya asilimia 40 umegharimu zaidi ya Sh Milioni 300.
Alipoulizwa zilipo fedha zingine za kukamilisha ujenzi wa bwalo hilo, mhandisi huyo alisema zilitumika kukamilisha miundombinu mingine ya shule hiyo, majibu yaliyomkasirisha Waziri Mkuu na kuuliza tena:
“Kwa nini fedha za bwalo zikafanye kazi nyingine tofauti na maelekezo ya serikali yanayoonesha kila jengo linatakiwa kujengwa kwa gharama yake iliyoainishwa.”
Akiuliza zilipo zaidi ya Sh Milioni 400 za ujenzi huo, sababu za bwalo hilo kutokamilika na wapi wanafunzi wa shule hiyo wanalia chakula; mhandisi huyo alikaa kimya akionekana hana majibu.
Akimuagiza mwanasheria wa serikali kuhakikisha wawili hao wanafikishwa mahakamani Waziri Mkuu alimtaka Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa kumtafuta popote alipo na kumrejesha Iringa aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kamendu ili naye aunganishwe katika kesi hiyo.
Aidha Waziri Mkuu amehoji sababu ya halmashauri hiyo kumlipa mkandarasi fedha zake zote pamoja na kwamba hajakamilisha sehemu ya ujenzi wa jengo la utawala, huku akitaka madawati yote katika shule hiyo yaliyotengenezwa chini ya kiwango, yaondolewe mara moja.