Manispaa ya Iringa yapata hati safi ripoti ya CAG
19 June 2024, 10:30 am
Wakati Mikoa mingine ikiwa na hati yenye mashaka kuhusu ukaguzi kwa hesabu za serikali, Manispaa ya Iringa imezidi kufanya vizuri katika hesabu zake kwa mwaka uliopita.
Na Adelphina Kutika
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Peter Serukamba amepongeza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa kupata Hati safi za Ukaguzi kwa hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni, 2022/2023.
Serukamba ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa Baraza Maalumu la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ya kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2022/23.
Aidha Serukamba ameiagiza halmashauri ya manispaa ya iringa kuwachukulia hatua za kisheria watumishi waliosababisha kuibuliwa kwa hoja zisizo za msingi katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) zinazohusu masuala ya ubadhirifu wa fedha.
Diwani wa kata ya Ruaha Tandes Sanga amemuomba mkuu wa Mkoa kutenga siku maalumu na kufanya Kikao cha ndani ili kujadili kwa kina hoja za CAG.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada amesema wamejipanga kuhakikisha wanafanya vikao vitakavyoleta suluhu ya utekelezaji bora wa miradi.
MWISHO