RC Serukamba apiga marufuku kuuzwa unga usiokuwa na virutubisho
21 May 2024, 11:12 am
Imeonekana kuwa mwelekeo wa kuchukua virutubisho umeongezeka kwa kiasi kikubwa miongoni mwa jamii ili kutokomeza udumavu mkoani Iringa.
Na Joyce Buganda
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Maafisa Elimu na Maafisa Biashara mkoani Iringa kuhakikisha unga unaouzwa kwa wananchi ni unga wenye virutubisho ikiwa ni moja ya mikakati ya kutokomeza udumavu unaotajwa kikithiri ndani ya mkoa wa Iringa.
Akizungumza katika kikao maalum cha kujadili masuala ya lishe bora kwa watoto na kutambulisha warutubishaji wa unga wa mahindi mkoani Iringa, Serukamba amesema katika mapambano ya udumavu mkoa wa Iringa ni vema shule zote wahakikishe wanatumia na kulima mahindi ya njano ili kupunguza udumavu kwa wanafunzi.
Aidha Afisa Mradi kutoka shirika la GAIN ambalo linajishughulisha kuweka virutubisho kwenye mahindi Dikson Minja amesema lengo ni kuwakutanisha wadau ili kujadiliana kwa pamoja namna ya kutokomeza udumavu kwa watoto.
Akizungumza kwa niaba ya walimu waliohudhulia kikao hicho mmoja wa walimu hao amesema ni vema wakuu wote wa shule kuweka mkakati wa kutopokea vyakula visivyo na virutubisho.