Vifaa vya milioni 100 kukuza sekta ya kilimo kwa vijana Iringa
20 May 2024, 8:52 pm
Katika kuhakikisha vijana wanaingia kwenye kilimo, zaidi ya shilingi milioni 100 zimetengwa ili kuongeza thamani ya sekta hiyo kwa mkoa wa Iringa.
Na Aadelphina Kutika
Vijana wapatao hamsini (50) mkoani Iringa wamekabidhiwa vifaa vyenye thamani ya shilingi millioni 100 ikiwa ni mpango wa kuwasaidia vijana wanaofanya biashara katika mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo ili kusaidia uzalishaji wenye tija .
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo iliyoandaliwa na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania TWCC, Mkuunwa Wilaya ya Iringa Kheri James ameeleza kuwa vifaa hivyo vitawasaidia vijana wafanyabiashara kuongeza uzalishaji wenye tija utakaowawezesha kushindana katika soko la kitaifa na kimataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC Bi. Mwajuma Hamza ameeleza kuwa kabla ya kuwapatia vifaa hivyo, wamefanikiwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa vijana yaliyojikita katika urasimishaji biashara, utaalam katika kilimo, ufugaji na programu za ulezi biashara.
Peter Mo ni Meneja wa Fedha kutoka kampuni ya Pass Leasing Tanzania amesema kwa kipindi cha miaka mitatu wamefanikiwa kuwafikia wakulima na wafanyabiashara wa kilimo wapatao 1,000 na kutoa vifaa vya kilimo vyenye thamani ya shilingi bilioni 50.
Kwa upande wao vijana wamesema kuwa vifaa walivyokabidhiwa ni mashine za kuvuta maji kwa ajili ya kilimo, mashine za kusaga, majokofu ambavyo vitawasaidia kuendesha shughuli zao ili kuondokana na wimbi la umaskini.
Hafla hiyo imehudhuriwa pia na viongozi kutoka TWCC, Pass Leasing Company, USAID, PASS, SIDO na wawakilishi wa halmashauri za mkoa wa Iringa.