Mafinga mji kuongeza ukusanyaji mapato
12 April 2024, 10:01 am
Licha ya Mafinga kuwa kinara katika ukusanyaji wa mapato, Bado Viongozi wa Halmashauri hiyo wamekuwa mstari wa mbele kupata Elimu namna ya kuboresha ukusanyaji wa mapato.
Na Hafidh Ally & Sima Bingilek
Halmashauri ya Mji Mafinga imepanga kuongeza kasi katika ukusanyaji wa mapato ili kupandisha uchumi na kuongeza ubora wa huduma za kijamii kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na baadhi ya Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Mji Mafinga kwenye ziara ya Mafunzo katika Halmashauri ya Mji Tunduma ambapo lengo la ziara hiyo ya Wataalamu na Waheshimiwa Madiwani ni Kujifunza namna ya Uendeshaji Shule za Mchepuo wa Kiingereza, Ukusanyaji wa Mapato hasa kwenye Maegesho ya Malori, ukusanyaji wa ushuru wa Maegesho, Leseni za biashara,stendi ya mabasi, uendeshaji wa vibanda vya masoko na uendeshaji wa masoko ya mazao.
“Hakika ziara hii imekuwa ya mafanikio makubwa kwani kile tulichokilenga kujifunza tumekipata sasa ni kwenda kuweka bajeti na kutekeleza hasa maegesho ya maroli na ukusanyaji wa mapato na uendeshaji wa shule za Mchepuo wa kiingereza.
Akizungumza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi. Fidelica Myovella amesema kiu kubwa ya Halmashauri ni kuona tunabuni Miradi Mikubwa ya ukusanyaji wa Mapato na kutoa huduma bora kwa wananchi wa Mji Mafinga na Watanzania kwa ujumla.
“ Kama hakuna Mapato hatuwezi kutoa huduma bora, tumekuja kujifunza ili tukirudi kukaweke mikakati na bajeti na kubuni vyanzo vikubwa vya mapato na kuboresha hali ya utoaji wa Huduma kwa wananchi” Fidelica Myovella Mkurugenzi Mji Mafinga.
Aidha Mheshimiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga kwa niamba ya waheshimiwa amesema ziara imekuwa ya mafanikio makubwa kwa kuwa mambo ambayo walikusudia kujifunza wamepata nafasi ya kuyaona na kupata maelezo kwa udani.
Soko la Mazao la kimataifa ni moja ya funzo kubwa kwetu kwani tumeona ukusanyaji wa mazao, ushuru na namna halmmashauri inafanya kupata ushuru kutoka kwa wakulima na ambavyo soko linatoa huduma kwa wakulima wote.
Ziara ya Mafunzo imehudhuriwa na waheshimiwa Madiwani kutoka Mji Mafinga, baadhi ya wataalamu na Afisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi.