Iringa kuzindua mkakati wa kukabili udumavu
4 March 2024, 12:24 pm
Licha ya takwimu kuonesha kuwa hali ya udumavu nchini imepungua hadi kufikia asilimia 30 mwaka 2022, bado mikoa ya Iringa na Njombe ina hali ya udumavu wa kutisha.
Na Frank Leonard
Wakati baadhi ya wadau wakionekana kutoziafiki takwimu zinazoonesha mkoa wa Iringa unaongoza kwa udumavu nchini, mkoa huo umetangaza kuyatumia maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mwaka huu kuzindua mkakati wake wa miaka mitano wa kukabiliana na changamoto hiyo.
Akitoa taarifa hiyo kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2023, Mkuu wa Mkoa alisema; “Takwimu za udumavu nchini zinaonesha mkoa wa Iringa unaongoza kwa kuwa na asilimia 59.6 ya watoto chini ya miaka mitano wenye udumavu.”
Mkoa wa Iringa unafuatiwa na mkoa wa Njombe wenye asilimia 50.4 na Rukwa wenye asilimia 49.8 pamoja na kwamba ripoti ya utafiti wa Hali ya Uzazi ya Afya ya Mama na Mtoto na Malaria inaonesha kuwa hali ya udumavu nchini imepungua hadi asilimia 30 mwaka 2022.
“Hii maana yake kwa kila watoto 10 mkoani mwetu, wastani wa watoto sita wana udumavu. Tunakuja na mkakati wa miaka mitano wa kukabiliana na changamoto hii. Tunaomba wadau wote mtuunge mkono katika kutekeleza mkakati huo,” alisema.
Mkuu wa Mkoa alisema mkakati wa kukabiliana na udumavu utahusisha utoaji wa elimu ya lishe bora, matumizi ya vyakula vyenye lishe bora kwa wanawake wajawazito na watoto, upatikanaji wa maji safi na salama, na ufuatiliaji wa maendeleo ya watoto.
Mengine ni pamoja na uwekezaji katika kilimo bora ili kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye lishe bora, kuendesha kampeni zinazohusiana na afya na udumavu ili kuongeza uelewa, kuboresha hali ya maisha ya wanawake na kushughulikia sababu za kijamii na kiuchumi.
“Tusikubali kubaki nyuma wakati uwezo wa kusadia watoto wetu tunao. mkakati tunaokwenda kuuzindua Machi 8 mwaka huu utahusisha wazazi, walezi, walimu, wataalamu wa afya, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla,” alisema.
Hata hivyo baadhi ya wadau akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Steven Mhapa wamehoji sababu za mkoa wa Iringa kuongoza kwa takwimu hiyo huku ripoti nyingine za mendeleo ya mtoto zikionesha hali tofauti.
Kama watoto wanaougua udumavu wanaweza kukabiliwa na ucheleweshaji wa maendeleo ya akili na kimwili na kuathiri uwezo wao wa kujifunza shuleni, Mahapa aliuliza, inawezekanaje watoto hao wakawa na ufaulu mzuri katika mitihani yao mbalimbali.
Akizungumzia mafanikio ya jumla katika utekelezaji wa mkataba huo, Ofisa Lishe wa Mkoa wa Iringa Anna Nombo alisema kumekuwa na mwitikio wa mkubwa wa viongozi wa ngazi zote katika kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa mkataba jambo linalotoa mwelekeo chanya wa utekelezaji wa viashiria vyake.
Kwa kupitia kiashiria cha matone ya Vitamini A alisema zaidi ya watoto 57,000 walifikiwa katika kipindi hicho na kati yao, watoto 248 waligundulika kuwa na utapiamlo mkali, 245 walipatiwa matibabu na kupona huku watatu wakifariki dunia.