Nuru FM
Nuru FM
2 April 2026, 09:26

Wagonjwa hao watapatiwa matibabu na upasuaji bure kwa asilimia 100 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa
Hafidh Ally
Wananchi wa Halmashauri ya Mji Mafinga wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya macho kupitia kliniki maalum ya madaktari bingwa ili kuimarisha afya ya macho kwa jamii na kusaidia wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka.
Akizungumza wakati wa zoezi la kupima macho kwa wagonjwa waliojitokeza katika Katika Hospitali ya Mji wa Mafinga, Meneja wa Mradi wa KCCO kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Steven Marwa amesema kuwa kliniki hiyo imefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 500 waliopata huduma ya uchunguzi wa macho na kati ya wagonjwa 82 waligundulika kuwa na tatizo la mtoto wa jicho.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Iringa, Dk. Jasmine Kachemela amewasema kuwa wananchi waliojitokeza katika Kliniki hiyo wengi wana changamoto ya Mtoto wa jicho na Uono hafifu huku akiwataka wananchi kufuata ushauri wa wataalamu wa afya mara wanapogundulika kuwa na matatizo ya macho.

Awali Mratibu wa Huduma za Macho katika Hospitali ya Mji Mafinga, Robert Michael Nganilevanu, amesema ameridhishwa na idadi kubwa ya Wananchi waliojitokeza kupata huduma hiyo hali inayoonesha kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa afya ya macho.
Hata hivyo baadhi ya wanufaika wa huduma hiyo, amewashukuru Madakari Bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa Kupita Mradi wa KCCO kwa kuwezesha huduma za uchunguzi na matibabu ya matatizo ya macho.
