Nuru FM
Nuru FM
2 April 2026, 08:43

Mzigo wa masomo magumu kwa watoto unaweza kuathiri ukuaji wao wa kiakili.
Na Adelphina Kutika
Wazazi na walezi katika Manispaa ya Iringa wamekumbushwa kuwa vituo vya kulelea watoto mchana havijaanzishwa kwa ajili ya kuwafundisha watoto masomo mazito, bali ni kwa ajili ya malezi ya awali yanayozingatia michezo na nyimbo ili kukuza akili zao bila kuwachosha.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, PJT MMMAM Mkoa wa Iringa, Martine Chuwa, katika kikao cha wamiliki wa vituo vya kulelea watoto mchana kilichoratibiwa na shirika la Idydc linalotetekeleza program ya Mtoto Kwanza awamu ya pili .
Chuwa ameeleza kuwa watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 4 wanapaswa kujifunza kupitia kuimba, kucheza na kushirikiana na wenzao, badala ya kubebeshwa mzigo wa masomo magumu ambao unaweza kuathiri ukuaji wao wa kiakili.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Iringa, Zaina Abasi Lean, amesema lengo la kikao hicho ni kuwajengea uelewa wamiliki wa vituo hivyo kuhusu malezi na makuzi ya awali ya mtoto pamoja na taratibu muhimu za kuanzisha na kuendesha vituo hivyo kwa kuzingatia miongozo iliyopo.
Baadhi ya wamiliki wa vituo vya kulelea watoto mchana walioshiriki kikao hicho wamesema wamepata maarifa muhimu, hususan namna ya kubaini watoto wenye changamoto za ulemavu unaoonekana na usioonekana, jambo ambalo hapo awali lilikuwa changamoto kubwa kwao.
