Nuru FM
Nuru FM
30 March 2026, 9:19 am

Na Fredrick Siwale
Uongozi wa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Upendo Yerusalemu kilichopo Halmashauri ya Mji Mafinga umewaomba wadau wa maendeleo kuwasaidia chombo cha usafiri kwa ajili ya kuwapeleka shule watoto hao.
Hayo yamezungumzwa na Mlezi wa kituo hicho Sista Dativa Msilu, wakati akipokea misaada ya kibinadamu kutoka kikundi cha wafanyabiashara wa Malimbichi cha Soko Kuu Mafinga na kuongeza kuwa watoto hao wamekuwa wakipitia adha ya usafiri kwani shule wanayosoma iko mbali kwa Km 6.

Kwa upande wake Sista Msaidizi Jema Mwilapwa amewashukuru wafanyabiashara hao kwa Moyo kuwafariji Watoto hao na kuomba wasichoke kusaidia wenye uhitaji.
Naye Mwenyekiti kikundi cha wafanyabiashara wa Malimbichi cha Soko Kuu Mafinga Julius Sanga (Polesa) amesema kuwa kikundi chao kimeamua kurejesha kwa jamii hasa kwa watoto hao ili kuwapa tabasamu.
Awali Katibu wa kikundi hicho Bi. Delfina Kipangula (Mama Lawelu) ameiomba Jamii kuendelea kuwa kuwasaidia Watoto Yatima na Waishio katika mazingira Magumu na hatarishi ili na wao wafurahie kama watoto wengine.
Kituo hicho chenye Jumla ya Watoto 29 ambao wanakabiliwa na changamoto ya umaliziaji wa ujenzi wa ukuta wa uzio ambao unajengwa kwa nguvu ya Wadau.
