Nuru FM
Nuru FM
24 March 2026, 9:12 am

Barabara hiyo ilihabirika kutokana na Mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Iringa.
Na Hafidh Ally
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Benjamin Sitta amewataka maafisa wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kushughulikia changamoto ya uharibifu wa miundombinu ya barabara katika Mtaa wa Kitasengwa, Kata ya Isakalilo, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ili kurejesha mawasiliano na shughuli za wananchi.
Mh. Sitta ametoa maagizo hayo mara baada ya kutembelea eneo hilo lililoathirika na kuongeza kuwa ni vyema Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, kupitia vikao vyake vya maendeleo, kuona umuhimu wa wa kutambua na kusajili barabara hizo ili kuiwezesha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuanza rasmi matengenezo ya miundombinu hiyo.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Barnabas Jabir amesema kuwa watashirikiana na wananchi wa eneo hilo kuhakikisha barabara hiyo inapitika.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Kitasengwa wameishukuru serikali ya Wilaya ya Iringa kwa kufika na kujionea hali ya barabara hiyo huku wakiiomba iweze kutatuliwa kwa ubora zaidi.
Katika siku za hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali yaliyopata madhara ya viwango tofauti kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika wilaya ya Iringa.
