Nuru FM
Nuru FM
17 March 2026, 9:55 am

Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa Kwa kishirikina na shirika la KCCO wanatoa huduma hizo za kibingwa kwa wananchi.
Na Hafidh Ally
Jumla ya wagonjwa 2,000 wamepata huduma ya matibabu ya macho mkoani Iringa katika kipindi cha Januari hadi Machi 2026 kutoka kwa madaktari bingwa wa macho wanaotoa huduma katika maeneo mbalimbali ya mkoa hapa.
Akizungumza wakati wa zoezi la kupima macho kwa wagonjwa waliojitokeza katika Kituo cha Afya Ipogolo, Manispaa ya Iringa, Meneja wa Mradi wa KCCO kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Steven Marwa amesema kati yao wagonjwa 200 wamefanyiwa upasuaji wa kutibu ugonjwa wa mtoto wa jicho.

Naye Daktari Bingwa wa Macho kutoka Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa Jasmine Kachemela amesema kuwa wamebaini magonjwa mbalimbali yanayohusisha uono hafifu kwa wananchi waliojitokeza katika kituo cha afya Ipogolo.
Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ipogolo Manispaa ya Iringa Musa Nurdin ameishukuru serikali kupitia wizara ya afya kwa kuwapatia madaktari bingwa katika kituo chao cha afya kwani imesaidia wananchi wengi wa ukanda huo kupata huduma za kibingwa kutoka kwa wataalamu wa afya.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma ya macho katika kituo hicho wameshukuru Uwepo wa kambi hiyo huku wakiwataka wananchi wenye matatizo ya macho kujitokeza kupata huduma hiyo ambayo hutolewa kwa gharama nafuu.
Shirika la KCCO linatekeleza huduma za matibabu ya macho mkoani Iringa kwa kipindi cha miaka mitatu na linalenga kuwafanyia upasuaji zaidi ya wagonjwa 5,000 wanaosumbuliwa na tatizo la mtoto wa jicho.
