Nuru FM
Nuru FM
13 March 2026, 12:30 pm

Watumishi wanapaswa kuzingatia ushirikiano katika maeneo yao ya kazi ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa.
Na Hafidh Ally
Watumishi wa umma wa kada mbalimbali ambao wamepata ajira mkoani Iringa wametakiwa kuzingatia misingi ya sheria za nchi, taratibu na miongozo ya kisheria ili kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa mkoa wa Iringa Kheri James wakati akizungumza na watumishi wa umma wapya 603 waliopata ajira katika taasisi mbalimbali za Serikali mkoani Iringa na kuongeza kuwa watumishi wa umma wanaotekeleza majukumu yao wanapaswa kuzingatia misingi ya utawala bora.
Amesema watumishi hao wana wajibu wa kuwa sehemu ya suluhisho la migogoro mbalimbali inayojitokeza katika jamii kupitia usimamizi wa haki, uwajibikaji na utoaji wa huduma kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi. Fidelica Myovela ameishukuru serikali kwa kuwapatia watumishi hao ambao watakuwa chachu ya kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi.