Nuru FM
Nuru FM
12 March 2026, 12:14 pm

“Kitendo cha kuwekwa kwa makufuli katika milango ya biashara zetu hatukubaliani nacho”
Na Fredrick siwale
Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Mafinga katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wamelalamikia hatua ya baadhi ya maafisa wa halmashauri hiyo kufunga milango ya maduka yao kwa madai ya kutolipa ushuru, wakidai kuwa hatua hiyo inaathiri na kudhoofisha shughuli zao za kibiashara.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara hao, Mwenyekiti wa Soko Kuu la Mafinga, Bwana Filinus Mgaya, amesema kuwa si vyema kwa maafisa wa halmashauri kumwaga vyakula vya wafanyabiashara pamoja na kufunga maduka yao, kwani hali hiyo husababisha hasara kubwa na kuharibu mitaji ya wafanyabiashara.

Aidha Mgaya amewataka wafanyabiashara kutokwepa wajibu wao wa kulipa kodi na ushuru wa Serikali na endapo mfanyabiashara anakumbana na changamoto za kifedha, ni muhimu kufuata utaratibu kwa kuwasiliana na mamlaka husika ili kufikia makubaliano ya kulipa ushuru huo kwa awamu badala ya kukwepa kabisa.
Kwa upande wake, Katibu wa Soko Kuu la Mafinga, Victor Mgani amekemea tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kuchelewa kufunga maduka yao kinyume na taratibu za soko.
Hata hivyo viongozi wa soko hilo wamewataka wafanyabiashara kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za biashara pamoja na kulipa kodi na ushuru kwa wakati, huku wakisisitiza umuhimu wa mazungumzo na ushirikiano kati ya wafanyabiashara na mamlaka za halmashauri ili kuepusha migogoro inayoweza kuathiri maendeleo ya biashara katika soko hilo.