Nuru FM
Nuru FM
11 March 2026, 9:09 am

Kutokana na changamoto ya ukosefu wa samani hizo, walimu walilazimika kutumia viti vya wanafunzi wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Na Ayoub Sanga
Mkurugenzi wa Ndete Store , Lucas Ndete, amekabidhi meza na viti kwa walimu wa Shule ya Sekondari Kimande iliyopo Kata ya Itunundu, Tarafa ya Pawaga, Wilaya ya Iringa, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa kwa uongozi wa shule hiyo.
Ahadi hiyo aliitoa alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuwapokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza (Welcome Form One) katika shule hiyo, ambapo Mkuu wa Shule aliwasilisha changamoto ya ukosefu wa meza na viti vya walimu.
Akizungumza wakati wa kukabishi samani hizo Ndete amesema kuwa sekta binafsi zina jukumu la kuunga mkono juhudi za Serikali katika miradi ya sekta mbalimbali inayogusa jamii huku akitoa wito kwa wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo kushirikiana na Serikali katika miradi ya kijamii ili kuchochea maendeleo .

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Kimande Mwl. Aloyce Mgongolwa ametoa shukrani kwa Mkurugenzi huyo kwa kutimiza ahadi yake, akisema kuwa msaada huo utasaidia kuondoa changamoto iliyokuwa ikiathiri walimu na hivyo kuboresha mazingira ya ufundishaji.
Naye Katibu wa Mafunzo, Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Anord Mvamba, ameipongeza Taasisi ya Ndete Store kwa kuchangia meza na viti kwa walimu wa Shule ya Sekondari Kimande iliyopo Kata ya Itunundu, Tarafa ya Pawaga, Wilaya ya Iringa, akisema mchango huo unasaidia kuboresha mazingira ya kufundishia.
Shule ya Sekondari Kimande ni shule mpya iliyojengwa katika Kata ya Itunundu, na ujenzi wake umegharimu takribani shilingi milioni 850, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi.
