Nuru FM
Nuru FM
5 March 2026, 5:16 pm

Mafunzo hayo yatasaidia kujua mfumo wa kupata takwimu halisi katika maendeleo ya ukuaji wa mtoto.
Na Adelphina Kutika
Waratibu wa afua tano zinazotekeleza mradi wa PJT–MMMAM katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wamepatiwa mafunzo ya siku moja kuhusu ujio wa Kadi ya Alama ya Malezi na Makuzi ya Mtoto (SCORECARD), mfumo mpya utakachosaidia kuboresha ufuatiliaji wa huduma za malezi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Akizungumza katika mafunzo yaliyoratibiwa na Mtoto kwanza mkoa wa Iringa Shirika la Developmentof Youth Disable and Children Care (IDYDC), Afisa Ustawi wa Jamii Hamza Shemweta muwezeshaji wa mafunzo, amesema lengo ni kuwajengea uwezo waratibu hao kuielewa kadi hiyo namna itakavyofanya kazi, kukusanya na kuchambua takwimu sahihi za watoto.

Kwa upande wake, Mratibu wa PJT–MMMAM Mkoa wa Iringa, Martine Chuwa, amesema ujio wa Kadi ya Alama umekuwa chachu ya kuboresha utoaji wa huduma kwa watoto na sasa wadau wataweza kujipima kwa kutumia takwimu sahihi na viwango vinavyoeleweka.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ikiwamo,Clous Kayombo Afisa Lishe kutoka Manispaa ya Iringa, amesema mafunzo hayo yameboresha utendaji kazi wao na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wataalamu wa sekta mbalimbali wanaohusika na malezi ya mtoto.
Hata hivyo uanzishwaji wa Kadi ya Alama ya Malezi na Makuzi ya Mtoto unatarajiwa kuleta mapinduzi katika ukusanyaji na matumizi ya takwimu, na hivyo kusaidia kupanga na kutekeleza mipango madhubuti ya kuboresha ustawi wa watoto.