Nuru FM
Nuru FM
6 February 2026, 12:54 pm

“Wananchi walilalamika kukosekana kwa mbolea ambayo imechukuliwa yote na wamiliki wa viwanda kinyume na taratibu”
Na Fredrick Siwale
Jumla ya Viwanda 7 vinavyochakata mazao ya Misitu Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa vimetozwa Faini ya shilingi Milion 15 kila moja kwa kutumia mbolea ya Ruzuku kama malighafi za viwanda vyao.
Hayo yamejiri mara baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dkt. Linda Salekwa kufanya ziara ya ukaguzi wa kushtukiza katika viwanda vya East Africa Zhen Yuan , Lush CHANZO, East Africa Born Wood , Yissen , Dhazong ambapo alibaini viwanda hivyo kutumia Mbolea hiyo ya Ruzuku ambayo Serikali imeelekeza itumike katika kilimo.
Dkt. Salekwa amesema kuwa walipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa na uhaba wa mbolea ambayo imehodhiwa na wamiliki wa viwanda hivyo ambavyo vinazitumia mbolea hizo kama malighafi za kutengeneza Gundi licha ya serikali kupunguza bei ya mbolea ili wakulima wanufaike na mpango huo.
“wote mnajua mkoa wa iringa umekuwa na changamoto ya udumavu, na serikali ilitaka wakulima wazalishe chakula kwa wingi kupitia mpango wa mbolea ya ruzuku na kuongeza uzalishaji wa chakula” Alisema Linda.

Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Samson Poneja ameipongeza serikali Wilaya ya Mufindi kwa kubaini changamoto hiyo ambapo amebainisha kuwa watawapa utaratibu wa kufuata baada viwanda hivyo kuonekana vina uhutiaji wa mbolea hiyo.
Awali Meneja wa NFRA Kanda ya nyanda za juu kusini Joshua Ng’ondya Amesema kuwa wamiliki wa viwanda hivyo watapaswa kulipa faini waliyopigwa ndani ya siku 14 huku Mamlaka hiyo ikihakikisha inawewezesha wadau hao na kuwarasimisha katika matumizi ya mbolea hiyo ili waweze kutumia katika viwanda vyao.
Akizungumza kwa niaba ya wamiliki wa Viwanda Wilaya ya Mufindi Bi, Fatuma Issa Kasairo alisema kuwa wamepokea maelekezo kutoka katika mamlaka husika na wameahidi kufuata hatua zote ili waweze kupata mbolea kwa utaratibu wa serikali.
