Nuru FM
Nuru FM
5 February 2026, 11:20 am

Kujiunga na bima ni hatua ya kujilinda na gharama zisizotarajiwa za matibabu.
Na Hafidh Ally
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James amewataka viongozi wa ngazi za vijiji na vitongoji kuwahamasisha wananchi wa maeneo yao kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya kwa uhakika.
Mh. Kheri ametoa Wito huo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo, akiwa katika Kituo cha Afya Magubike kilichopo Kata ya Nzihi, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na kuongeza kuwa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni mkakati muhimu wa serikali unaolenga kuhakikisha kila kaya inanufaika na huduma za afya kwa kuchangia shilingi 150,000/= kwa mwaka.
Mhe. Kheri amewaagiza wenyeviti wa vijiji na vitongoji, watendaji pamoja na madiwani kuhakikisha wanawatumia wataalamu wa Afya kutoa elimu juu ya umuhimu na faida za bima ya afya ili kila mwananchi aweze kujiunga na kunufaika na mpango huo.

Merisiana Josephati Ni mkazi wa Kijiji cha Ng’enza Wilaya ya Iringa amesema kuwa wakati serikali ikihamasisha wananchi kujiunga na mpango wa bima ya afya kwa wote ni vyema wakaboresha katika upatikanaji wa dawa.
Mpango wa Bima ya afya kwa wote unasaidia wananchi kupata huduma za afya kwa shilingi 150,000 kwa Kaya ya watu wasiozidi sita (6) itakayojumuisha mwanachama mchangiaji, mwenza wa mwanachama na wategemezi wanne (4).