Nuru FM
Nuru FM
15 January 2026, 11:08 am

“Mimi sipendi kuona miradi ya maendeleo inasimamiwa kwa kusuasua” RC Kheri
Na Ayoub Sanga
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James ameagiza kuimarishwa kwa ufuatiliaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Iringa ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Mhe. Kheri ametoa agizo hilo wakati wa ziara za ukaguzi wa miradi ya maendeleo Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, ambapo amebaini kusuasua kwa mradi wa ujenzi wa shule ya awali na msingi unatokelezwa kupitia shule ya Sekondari Ngwazi kutokana na ukosefu wa vifaa vya ujenzi hususani vigae, licha ya kuwepo kwa mafundi pamoja na fedha za utekelezaji wa mradi huo.

RC Kheri James amesema kuwa ni jambo lisilo na mantiki kuona mradi unakwama kwa kukosekana kwa vifaa ilhali fedha zipo na mafundi wapo tayari kufanya kazi.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa vifaa vyote vya ujenzi vinapatikana mara moja na miradi yote iliyokuwa imekwama kuanza kutekelezwa haraka sana.