Nuru FM
Nuru FM
10 January 2026, 4:31 pm

Ubovu wa kivuko hicho unawalazimu watoto na wakazi wengine kuvuka kwa tahadhari.
Na Hafidh Ally
Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Mh. Fadhili Fabiani Ngajilo ametoa siku 14 kuanzia leo Jan 10 2026 kwa Mtendaji wa Kata kushirikiana na Ofisi yake kuhakikisha wanakarabati Kivuko cha TARO kilichopo Mtaa wa Ngeleli Kata ya Ruaha Manispaa ya Iringa.
Ngajilo ametoa kauli hiyo leo mara baaada ya kufanya ziara ya kikazi katika Kata hiyo ambapo alifika na kujionea hali halisi katika Kivuko hicho ambacho kimekuwa kibovu jambo linalohatyaraisha usalama wa wananchi wa mtaa huo.
“Ninamuagiza Mtendaji wa Kata kushirikiana na Katibu wa Ofisi ya Mbunge kushughulikia suala hilo haraka sana ndani ya siku 14 wananchi waweze kutumia kivuko hiki kama daraja la kiwango kizuri, kwani serikali ya awamu ya Sita inataka wananachi wake wake na tabasamu”
Ngajilo amesema kuwa atahakikisha miundombinu ya Kivuko hicho inakuwa bora na wananchi wanavuka bila kikwazo chochote na kuendelea kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ruaha Musa Salum Mbungu amesema kuwa ubovu wa kivuko hicho imekuwa ni changamoto ya muda mrefu hasa kwa wanafunzi wanaovuka kwenda shule hasa kipindi cha mvua kunakuwa hakuna usalama kabisa.
“Kwanza tunamshukuru Mbunge wetu kwa kuja na kutatua changamoto hii ya kivuko kwani kimeshaleta madhara kwa wananchi na kuna mwananchi mmoja alidongoka na kuvunjika mguu na sasa anaendelea na matibabu na mnaweza hata kwenda kumwona”alisema Mbungu.

Awali Wananchi wa Mtaa wa Ngeleli uliopo Kata ya Ruaha Manispaa ya Iringa wamesema kuwa ubovu wa kivuko cha TARO (TARI) ambacho kinatenganisha wakazi wa eneo hilo na Mitaa jirani umeleta athari kwa wananchi wanaovuka kwenda kulima, na wanafunzi kuzunguka umbali mrefu kwenda shule.